Kocha Mkuu wa Yanga, Nesreddine Nabi amewaangalia wapinzani wao, Namungo FC na kusema wanahitaji kujiweka fiti zaidi kuhakikisha wanafanikiwa kupata pointi tatu katika mchezo dhidi yao wa Ligi Kuu Tanzania Bara
Nabi aliyeshinda tuzo ya kocha bora wa ligi kuu msimu huu mara mbili, amesema hakuna mechi iliyokuwa rahisi mbele yao hasa wanapokwenda kukutana na timu ambayo iliwasumbua katika mzunguko wa kwanza.
Alisema katika mechi ya kwanza walitoka sare ya 1-1 wakiwa ugenini, ana imani watakuwa wamebadilika kwa sababu wamefanya mabadiliko benchi la ufundi na kuwa na kiwango bora zaidi.
"Namungo FC ina wachezaji wazuri ukiangalia benchi la ufundi tofauti na mechi ya kwanza, tunatakiwa kujiandaa kuhakikisha tunafikia malengo yetu ya kupata pointi muhimu katika michezo iliyopo mbele yetu"
"Kazi kubwa kwa sasa kuendelea ni kujiimarisha zaidi kila nafasi ukiangalia katika mechi iliyopita kuna baadhi ya wachezaji akiwemo Saido Ntibanzokiza na Fiston Mayele kucheza wakiwa wagonjwa," alisema Nabi
Yanga tayari imeanza mazoezi kujiandaa na mchezo huo ambao utapigwa Jumamosi ijayo, April 23 katika uwanja wa Benjamin Mkapa
Habari njema kwa mashabiki wa Yanga ni kurejea kikosini kwa wachezaji kadhaa ambao walikuwa majeruhi
Wachezaji waliorejea ni Khalid Aucho, Chico Ushindi, Jesus Moloko na Farid Mussa huku Feisal Salum na Yacouba Songne wakiendelea na mazoezi chini ya uangalizi