Kiungo mshambuliaji wa Yanga Saido Ntibazonkiza amesema wameuchukulia kwa uzito mkubwa mchezo wa ligi kuu dhidi ya Namungo Fc ambao utapigwa kesho Jumamosi katika uwanja wa Benjamin Mkapa
Saido ambaye msimu huu amefunga mabao sita kwenye ligi na kutoa pasi nne za mabao, amesema kila mchezo kwao ni kama fainali hivyo wamefanya maandalizi kikamilifu huku wakifahamu wanakutana na timu nzuri
"Kwetu kila mechi ni kama fainali hivyo tumejiandaa vyema kuhakikisha tunaweza kupata matokeo. Nafahamu mchezo hautakuwa mwepesi, Namungo Fc tulicheza nao duru ya kwanza na tukatoka sare. Sasa tutakuwa katika uwanja wetu wa nyumbani hivyo tutapambana kuhakikisha tunashinda," alisema Saido
Mchezo huo ambao utapigwa kuanzia saa moja usiku, huenda ukashuhudia baadhi ya wachezaji waliokuwa majeruhi wa muda mrefu katika kikosi cha Yanga wakirejea
Kwa mara ya kwanza baada ya miezi kadhaa, Yanga imefanya mazoezi ikiwa na wachezaji wake wote
Mabingwa hao wa kihistoria walichimbia kambini Avic Town wiki nzima kujiandaa na mchezo huo