Alama tatu zimebaki jijini Dar es salaam kwa Yanga kupata ushindi wa kwanza dhidi ya Namungo Fc katika mchezo mkali uliopigwa uwanja wa Benjamin Mkapa
Fiston Mayele ameendeleza moto wake wa kutetema, akifunga bao lake la 12 msimu huu akiipa uongozi Yanga kwenye dakika ya 17
Shiza Kichuya akairejesha Namungo Fc mchezoni kwenye dakika ya 33 akifunga kwa shuti la mbali, akipokea pasi kutoka kwa Lucas Kikoti
Kabla ya kufungwa kwa bao hilo ilionekana mshambuliaji wa Yanga Mayele alifanyiwa madhambi lakini mwamuzi Arajiga akapeta
Krosi murua kutoka kwa Khalid Aucho ilitua mguuni kwa Feisal Salum 'Fei Toto' ambaye aliifungia Yanga bao la pili kwenye dakika ya 38
Yanga itabidi wajilaumu wenyewe kwa kushindwa kupata ushindi mnono katika mchezo huo kwani walikosa nafasi nyingi za wazi
Ni ushindi ambao umemfunga mdomo kocha msaidizi wa Namungo Fc Jamhuri Kiwhelo ambaye baada ya Namungo kusawazisha aliwadhihaki mashabiki wa Yanga kwa staili yake ya kushangilia
Ni alama tatu muhimu kwa Yanga ambayo sasa inaendelea kuukaribia ubingwa, wakifikisha alama 54 na kujikita kileleni mwa msimamo wa ligi kwa tofauti ya alama 13
Mchezo unaofuata ni dhidi ya Simba, April 30






