Msemaji wa Yanga Haji Manara amesisitiza kuwa ili waweze kuwa mabingwa wa ligi kuu msimu huu, hesabu ya alama zao inapaswa kuwa haiwezi kufikiwa na timu nyingine 15 zinazoshiriki ligi kuu msimu huu
Akizungumza mapema leo, Manara alisema kwa sasa Yanga ina faida ya alama 13 kileleni mwa msimamo wa ligi lakini haziwapi uhalali wa kuanza kusherehekea ubingwa kwa kuwa bado hawajatwaa ubingwa huo
"Nimelisema hili mara nyingi ili mashabiki wetu waelewe, sisi tunaongoza ligi kwa tofauti ya alama 13 lakini bado hatujashinda ubingwa. Ili uweze kuwa bingwa unapaswa kukusanya alama nyingi kuliko timu zote zinazoshiriki ligi"
"Mpaka sasa bado hatujakusanya alama nyingi ambazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine zote, hivyo bado tuko kwenye mapambano ya kuwania ubingwa"
"Kinachotupa imani ni ubora wa kikosi chetu, kama tutaendelea kucheza hivi katika michezo 10 iliyobaki, tunaweza kufanikisha malengo yetu," alisema Manara
Akizungumzia mchezo wa Jumamosi dhidi ya Simba, Manara amesema Yanga itawaheshimu wapinzani wao lakini dhamira waliyonayo ni kushinda mchezo huo
Katika hatua nyingine Manara amewataka mashabiki kununua tiketi mapema kwani siku ya mchezo hakutakuwa na tiketi zitakazouzwa
"Uongozi, Bodi ya Ligi pamoja na N-Card tumekubaliana, hakutakuwa na mauzo ya tiketi Jumamosi siku ya mchezo, ndio maana tumeanza kuuza tiketi mapema siku ya jana. Hivyo tunawaomba mnunue tiketi mapema. Tungependa kuona kila mashabiki watatu wanaoingia uwanjani, wawili ni Yanga"Β