Zikiwa zimebaki siku tano kabla miamba ya soka nchini Yanga na Simba kuchuana kwenye mchezo wa raundi ya pili wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi amesema wamejiandaa vyema kuhakikisha wanashinda mchezo huo.
Nabi hatakuwepo kwenye benchi la Yanga kwenye mchezo huo kutokana na adhabu ya kadi nyekundu aliyoipata kwenye mchezo wa robo fainali wa Kombe la FA dhidi ya Geita FC, lakini kocha huyo raia wa Tunisia amesema ili kufanikisha malengo yao, wanapaswa kutumia vyema kila nafasi wanayotengeneza pamoja na kupunguza makosa katika safu ya ulinzi
Nabi aliyepachikwa sifa ya Profesa kutokana na umahiri wake, amesema pamoja na matokeo ya ushindi wanayoyapata kwenye ligi, lakini mchezo huo wa Jumamosi ni mgumu sababu wanakwenda kucheza na timu kubwa yenye wachezaji bora na wenye uzoefu, hivyo ukifanya makosa ni vigumu kukuacha salama.
"Tupo katika maandalizi kabambe kuelekea mchezo dhidi ya Simba, sababu lengo letu la kwanza ni kushinda, lakini hatutaweza kufanikiwa kama hatutopunguza makosa"
"Tunapaswa kutumia vizuri nafasi tunazotengeneza na safu yetu ya ulinzi kutofanya makosa sababu Simba ni timu kubwa ina wachezaji wanaojitambua," alisema Nabi
Jumamosi katika mchezo wa ligi kuu dhidi ya Namungo Fc, Yanga ilikosa nafasi nyingi za wazi jambo ambalo Nabi amesema hataki kuliona kwenye mchezo dhidi ya Simba
Pamoja na kupata ushindi wa mabao 2-1 kwenye mchezo huo, kocha msaidizi Cedric Kaze alisema baada ya mchezo kuwa walipaswa kupata ushindi wa kuanzia mabao matano kwa nafasi ambazo walikosa