Nahodha wa Yanga, Bakari Mwamnyeto amewataka wachezaji wenzake kuongeza mapambano ili kutimiza lengo lao la kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.
Mwamnyeto amesema matokeo ya sare katika michezo mitatu iliyopita yasiwavunje moyo bado wanapaswa kuongeza juhudi katika kila mechi zilizobaki ili kurudi kwenye mwenendo wao walioanza nao msimu huu.
"Inawezekana ni uchovu sababu hivi karibuni tumecheza mfululizo, lakini hiyo haipaswi kuwa sababu ya msingi itakayotufanya kupoteza ubingwa kitu cha msingi ni sisi wachezaji tuongeze juhudi kwenye mechi zetu zilizobaki ili kutimiza malengo ambayo ni ubingwa" alisema Mwamnyeto
Nahodha huyo ambaye yupo katika harakati za kusaini mkataba mpya wa kuendelea kuitumikia timu hiyo, alisema kwa sasa kila mchezaji amepewa majukumu yake ya kufanya na anamiini kwa kutimiza hilo litasaidia kuhakikisha walichokikusudia wanakitimiza.
Mwamnyeto amesema pamoja na presha kuwa kubwa kwao lakini kwa ubora wa kikosi chao bado wanayo nafasi ya kufanya vizuri kwenye mechi hizo saba zilizo salia ispokuwa kitu cha msingi ni wao kutimiza malengo yao na mashabiki wao kuendelea kuwapa sapoti
Mwamnyeto alisema Yanga ni timu kubwa na msimu huu umekuwa na mafanikio makubwa kwao, hivyo haitapendeza kama watalikosa taji hilo ndio maana yeye akiwa kama kiongozi wa wachezaji amewaomba wenzake kuendeleza kasi waliyoanza nayo msimu huu