Makamu Mwenyekiti wa Yanga Fredrick Mwakalebela amekiri kuwa mabingwa hao wa kihistoria wamemuulizia mshambuliaji anayecheza kwa mkopo USGN ya Niger Victorien Adebayor
Adebayor ni mchezaji wa HB Koge ya Denmark akiwa ametolewa kwa mkopo kuitumikia USGN ambayo ilikuwa kundi moja ya Simba katika michuano ya kombe la Shirikisho barani Afrika
Licha ya kusambaa kwa taarifa kuwa klabu ya Simba tayari imemalizana na nyota huyo aliyefunga mabao sita hatua ya makundi ya michuano ya kombe la Shirikisho, Mwakalebela amesema hakuna ukweli wowote kwani hata Yanga inamuwania mchezaji huyo
"Wanasema wamemsajili waambie waonyeshe hata mkataba wa awali waliosaini nae. Huwezi kusema mchezaji ni wako wakati hata mkataba hauna"
"Nikuhakikishie Yanga tumeongea na Adebayor, yule bado sio mchezaji wa Simba, kama wameshamalizana nae waoneshe basi mkataba wa awali, hata sisi tunaweza kumchukua," alisema Mwakalebela katika mahojiano na TV3
Yanga tayari imejihakikishia kucheza michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika msimu ujao, Wananchi wakiwa wameanza maboresho ya kikosi
Kiungo mshambuliaji wa Asec Mimosas Stephen Aziz Ki raia wa Burkina Faso na mlinzi wa kushoto Mustafa Kizza raia wa Uganda ni miongoni mwa wachezaji wanaotajwa kuwa kwenye mipango ya Yanga