Kaimu Mtendaji Mkuu wa Yanga Senzo Mazingisa amesema wamepokea kwa mikono miwili shindano la NANI ZAIDI iliyoanzishwa na Azam Media ambalo itawahusisha mashabiki watimu zote kuzipigia kura timu zao kila kura ikiwa na thamani ya Tsh 1000/-
Akizungumza katika uzinduzi wa Shindano hilo, Senzo amesema utajiri wa mashabiki ambao klabu za Yanga na Simba wanao, unapaswa kuwa na faida kwa klabu hizo na sio kuishia katika kutaniana na kupiga kelele tu
"Nilipokuja Tanzania kwa mara ya kwanza, nilipoona wingi wa mashabiki wa klabu hizi, niliona ni fursa kubwa ya kiuchumi. Tutaendeleza upinzani wetu wa jadi na kutaniana kama kawaida lakini inapokuja fursa ya kiuchumi Yanga na Simba tunapaswa kushirikiana"
"Tumekuwa kwenye majadiliano na viongozi wa Simba, Azam Media na hata Serikali ili kuhakikisha jambo hili linafanikiwa. Sisi tunawataka mashabiki wetu waonyeshe kwa vitendo kuwa sisi ni zaidi kwa kupiga kura kwa wingi"
"Shindano hili halisimamishi mipango yetu mingine kama kusajili Wanachama, bali ni nyongeza ya kile ambacho tunafanya katika mchakato wetu wa Mabadiliko," alisema Senzo
Nae Msemaji wa Yanga Haji Manara amesema watafanya kampeni kubwa kuwahamasisha mashabiki ili waipigie klabu yao kura nyingi ambazo ni sawa na fedha zitazotumika katika mipango mbalimbali ya maendeleo ya klabu