Msimu uliopita mashabiki wa Yanga hawakuridhishwa na uamuzi wa kuuzwa kwa winga Tuisila Kisinda aliyesajiliwa na RS Berkane, mabingwa wa kombe la Shirikisho Barani Afrika msimu huu
Hata hivyo usajili makini uliofanywa chini ya wadhamini wao GSM, umewasahaulisha Wananchi kuhusu kuondoka kwa Kisinda na baadae Mukoko Tonombe aliyesajiliwa na TP Mazembe
Jambo moja la uhakika ni kuwa msimu ujao Wananchi nao watapenda kuona timu yao inafanya vizuri kwenye michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika
Katika dirisha la usajili ambalo litafunguliwa baada ya msimu kumalizika, wengi hawatarajii kuona Yanga ikiuza wachezaji wake muhimu zaidi ya kuongeza wachezaji wa kuboresha maeneo yenye mapungufu
Zipo tetesi kuwa RS Berkane wanaweza kurejea tena Jangwani safari hii wakimtaka nyota na kinara wa mabao Fiston Mayele
Hivi karibuni katika moja ya mahojiano yake, Florent Ibenge ambaye ni mkufunzi wa RS Berkane alieleza kushangazwa na uwezo anaoonyesha Mayele ambaye msimu uliopita alikuwa nae AS Vita
Kabla ya kutua Yanga, Mayele alikuwa sehemu ya kikosi cha AS Vita kilichotwaa ubingwa wa ligi kuu ya DR Congo chini ya Ibenge ambaye baada ya msimu kumalizika alitimkia RS Berkane huku Mayele akitua Yanga
Mayele alikuwa mfungaji bora wa AS Vita msimu uliopita akipachika mabao 14 na kushika nafasi ya pili katika orodha ya wafungaji bora wa ligi kuu ya DR Congo
Kwa mikakati ambayo Yanga wameiweka kuelekea msimu ujao, haitakuwa rahisi kumuachia Mayele aondoke kama walivyofanya kwa Kisinda