Klabu ya Yanga leo imetangaza mafanikio waliyopata katika mradi wa kusajili Wanachama uliaonza miezi sita iliyopita
Kilinet ambao ndio wataalam waliopewa jukumu la kusimamia kanzidata itakayobeba taarifa za Wanachama waliosajiliwa kidigitali, kupitia Mkurugenzi Mtendaji Mohammed Saleh, wametangaza kusajili Wanachama 34,650
Kupitia ada za Wanachama hao, Yanga imekusanya jumla ya Tsh Bilioni 1.07 na kufanya kuwa klabu ya kwanza katika ukanda wa Afrika Mashariki na kati kukusanya fedha nyingi kutoka kwa Wanachama
Yanga inatarajiwa kuanza awamu ya pili ya mradi huo hivi karibuni ambapo ni kusajili Mashabiki
Ili kusajiliwa kuwa shabiki unayetambuliwa na klabu, gharama yake ni Tsh 17,000/- wakati gharama ya usajiliwa kuwa Mwanachama ni Tsh 31,000/-
Kadi ya shabiki itakuwezesha kuingia uwanjani kushuhudia mechi mbalimbali pamoja na kupata punguzo la bei ya bidhaa zinazouzwa kwenye maduka washirika wa Yanga
Yanga imejiwekea malengo ya kusajili angalau mashabiki Milioni 1
Msemaji wa Yanga Haji Manara amesema kama klabu wana kila sababu ya kujivunia mafanikio yao, wamedhihirisha ukubwa wao kwa vitendo
"Tuna kila sababu ya kutamba na kujivunia mafanikio haya. Tunaposema Yanga ni kubwa tunamaanisha kwa mujibu wa takwimu. Kuna timu hapa katika kipindi cha miezi sita wamekusanya Milioni 60 wanaweza vipi kushindana na Yanga," alitamba Manara
Nae Mtendaji Mkuu wa Yanga Senzo Mazingisa amesema anajivunia mafanikio hayo waliyopata kusajili Wanachama kidigitali kwa ushirikiano na Kilinet
"Nipo hapa kama CEO najivunia sana kwa Klabu yangu kwa Jinsi tulivyofanikiwa kwenye hili zoezi la Usajili wa Kidigitali kwa kushirikiana na Kampuni ya Kilinet Afrika"