Msemaji wa Yanga Haji Manara amesema timu hiyo itasajili wachezaji wanne wa kigeni katika kikosi chao kuelekea msimu ujao
Akizungumza katika Mkutano na Wanahabari mapema leo, Manara amewataka mashabiki wa Yanga wasiingie kwenye mtego wa tetesi zisizo sahihi kwani wanafahamu wapo wachezaji vyombo vya habari vitaripoti wanatakiwa na Yanga ili pale watakaposajiliwa na Simba ionekane wamezidiwa katika usajili
"Wacha niwaambie taarifa kuhusu usajili wetu. Tumepanga kusajili wachezaji wanne tu wa Kimataifa, kama italazimu sana tutaongeza mchezaji mmoja"
"Nawatajia nchi ambazo wanatoka wachezaji hao, mmoja anacheza ligi kuu ya Ivory Coast, mwingine anacheza ligi kuu ya Angola. Mmoja alikuwa akicheza ligi kuu ya Afrika Kusini na mwingine alikuwa akicheza ligi hapa Afrika Mashariki lakini sijui ni nchi gani," alidokeza Manara
Kuhusu usajili wa wachezaji wa ndani, Manara amesema hawatarajiwi kuongeza mchezaji mwingine benchi la ufundi limeridhika na wachezaji wa ndani waliopo
"Tunao wachezaji ambao tayari wamezoeana na wenzao na wamezoea mazingira hatuwezi kumsajili mchezaji eti kwa sababu alitufunga au anapiga sana chenga"
Wachezaji ambao ni wazi watajiunga na Yanga ni Stephane Aziz Ki (Asec Mimosas-Ivory Coast), Lazarus Kambole (Kaizer Chiefs - Afrika Kusini), Lomalisa Mutambala (Sagrada Esperanca - Angola) na Bernard Morrison? (Afrika Mashariki)