Kocha Msaidizi wa Yanga Cedric Kaze amesema wako tayari kwa mchezo wa ligi kuu dhidi ya Polisi Tanzania ambao utapigwa kesho Jumatano katika uwanja wa Benjamin Mkapa
Mchezo huo ni wa mwisho kwa Yanga kucheza katika uwanja wa Benjamin Mkapa msimu huu, mchezo wao dhidi ya Mtibwa Sugar wameupeleka uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha
Akizungumzia maandalizi kuelekea mchezo huo, Kaze amesema licha ya kuwa tayari wametwaa ubingwa, wamedhamiria kuwaaga mashabiki wao wa jijini Dar es salaam kwa kupata ushindi mnono
Kaze amesema wanatambua uwezo wa Polisi Tanzania kwani licha ya kuwa walipata ushindi katika mchezo wa kwanza uliopigwa uwanja wa Sheikh Amri Abeid, mchezo ulikuwa mgumu
"Ni mchezo muhimu kwetu ambao tunahitaji ushindi. Ni mchezo wa kwanza tangu tulipotwaa ubingwa lakini tunacheza katika uwanja wetu wa nyumbani kwa mara ya mwisho msimu huu hivyo tutahitaji kuwapa furaha mashabiki wetu kwa kupata ushindi"
"Tunafahamu Polisi Tanzania ni timu nzuri, tulicheza nao Arusha na walitupa ushindani lakini tunaamini tutaweza kufanya vizuri zaidi katika mchezo huu unaochezwa uwanja wa Mkapa," alisema Kaze