Msemaji wa Yanga Haji Manara amemuomba radhi Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Wallace Karia kwa tukio lililotokea mkoani Arusha kwenye mchezo wa fainali kombe la Shirikisho la Azam kati ya Yanga dhidi ya Coastal Union
Manara amesema pamoja na kuwaomba radhi wanafamilia wa soka Tanzania, kipekee amemuomba radhi Karia na zaidi alikwenda nyumbani kwake kumuona
"Nikiwa uwanjani, mimi hupenda kukaa karibu na mashabiki, Muda ule mashabiki walikuwa wakinipigia kelele, na mimi nina presha ya mechi, hapo tumeshafungwa goli moja, muda huo nikapanga kuondoka ikifika half time, nikawaambia wenzangu tuondoke"
"Ghafla nikasikia sauti ya Rais, na alinijia kwa ukali, kwangu kutokana na temple ya mechi nikashindwa kujizuia, lakini sikumtamkia tusi, akaniambia ondoka, Nikamwambia hii sio sawa kunifokea, tukaanza kuzozana, basi ikabidi niondoke"
"Jana nikaenda nyumbani kwa Rais Wallace Karia nikamuomba msamaha, na mimi naomba msamaha kwenu familia ya mpira wa Tanzania"
"Hata kama yeye ndiye alinianza lakini naomba msamaha, kwa namna yoyote ile nilikosea kujibizana na Rais wa mpira. Kama itaonekana nastahili kuchukuliwa hatua nipo tayari kupokea adhabu hiyo, lakini lazima niombe msamaha bila kujali kamati itaamua nini," amesema Manara