Mtendaji Mkuu wa Yanga Senzo Mazingisa amesema msimu ujao wamedhamiria na watahakikisha wanatinga hatua ya makundi ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika
Baada ya kutwaa ubingwa wa ligi kuu pasipo kupoteza mchezo, Yanga imejihakikishia tiketi ya kushiriki ligi ya mabingwa, michuano ambayo walitolewa katika hatua za awali msimu uliopita
Senzo amesema hawatarudia makosa yaliyojitokeza katika msimu uliopita ambapo walikosa maandalizi ya kutosha
"Msimu uliopita tulikumbana na changamoto nyingi zilizosababisha tukakosa muda mzuri wa kufanya maandalizi. Tumejipanga, tunawaahidi mashabiki wetu, tutapambana ili tufike hatua ya makundi"
"Hatutakuwa na changamoto ya kuwakosa wachezaji wetu wapya kwani usajili wao utakamilishwa kwa wakati na kupata vibali vyao mapema"
"Tutakuwa na kambi nzuri ambayo itawapa wachezaji na benchi la ufundi muda mzuri wa kujiandaa," alisema Senzo
Michuano ya ligi ya mabingwa inatarajiwa kuanza mwezi Septemba ambapo mechi za hatua ya awali zitapigwa kati ya Septemba 9-11