Jana Yanga ilitangaza rasmi kuachana na wachezaji wawili wa kigeni ili kukidhi matakwa ya kanuni za usajili wa ndani ambapo ni wachezaji 12 tu wanaoruhusiwa kusajiliwa
Ni Chico Ushindi na Yacouba Songne ambaye hata hivyo Yanga imeweka bayana itazungumza nae ili kuona wanamsaidia vipi wakati huu ambao mkataba wake umemalizika na bado anahitaji kuimarika kutokana na majeraha makubwa aliyopata mwezi Novemba 2021
Kuna maoni tofauti miongoni mwa mashabiki wa Yanga ambapo wapo ambao hawajaridhishwa na kuachwa kwa Ushindi ambae anarejea katika klabu yake ya zamani, TP Mazembe
Ushindi 'uliuwasha' moto kwelikweli katika michezo ya mwishoni msimu uliopita akifunga mabao mawili na kutoa pasi moja ya bao
Tangu alipotua Yanga mwezi Januari 2022, Ushindi alishiriki katika michezo 10 na hakuna mchezo wowote ambao alicheza dakika 90
Changamoto ambayo pengine imepelekea benchi la ufundi kupendekeza aachwe, ni majeraha
Ushindi alikuwa akikabiliwa na mfululizo wa majeraha, haikuwa rahisi kwake kutumika katika mechi mfululizo
Atacheza mechi moja atakosekana katika michezo mitatu, minne n.k halafu ataonekana tena uwanjani
Yanga ina malengo makubwa msimu ujao, kutetea mataji yote matatu na kufanya vizuri kwenye michuano ya ligi ya mabingwa ambapo Wananchi wanataka angalau kutinga hatua ya makundi
Isingekuwa rahisi kwa Ushindi kujumuishwa katika kikosi licha ya ubora alioonyesha katika michezo ya mwisho
Ni sababu ya majeraha ambayo pia imechangia Yacouba kuenguliwa kikosini. Ni wazi Yacouba atahitaji muda zaidi kabla ya kurejea uwanjani akiwa timamu
Yanga imeamua kubaki na wachezaji 12 wa kigeni ambao hawana rekodi mbaya ya majeraha na wanaweza kutumika kwa dakika nyingi
Ni wazi, uamuzi wa kuachana na Saido Ntibazonkiza pia ulizingatia mahitaji hayo ya timu