Kocha Mkuu wa Yanga, Nesreddine Nabi amesema nidhamu na kujituma kwa kila wachezaji wake ndio kitu anachohitaji kukiona ambacho kitasaidia kutetea mataji waliyobeba msimu uliopita, lakini itawasaidia kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika
Kikosi cha Yanga kinaingia kambini leo huku Nabi ambaye alikuwa kwao kwa mapumziko akitarajiwa kurejea nchini leo na kuelekea moja kwa moja Avic Town, Kigamboni ili kuanza rasmi maandalizi ya msimu mpya wa 2022/2023.
Nabi amesisitiza kuwa hakutakuwa na mabadiliko kwenye usimamizi wa nidhamu kwani ni muhimu kwa wachezaji wake kuwa na nidhamu ili kuhakikisha wanatekeleza majukumu atakayowapa.
Wakati wa mapumziko, Nabi alitoa programu kwa wachezaji wake wa zamani na wapya waliosajiliwa ili kuanza mazoezi ya kuiandaa miili yao kuwa fiti na yenye utimamu.
"Usajili ni mzuri niwapongeze uongozi katika kusajili kulingana na mapendekezo na mahitaji ya timu pamoja na mashindano yaliyopo mbele yetu"
"Msimu mpya hautakuwa rahisi kwa sababu ya usajili uliofanywa na timu nyingine, pia ukizingatia tunaenda kushiriki michuano ya CAF tunatakiwa kuwa imara na kufika hatua ya robo fainali, hatuwezi kufika huko lazima tuwe na hali ya nidhamu na kujituma katika kila mechi," alisema Nabi.
Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli, amesema tayari idadi kubwa ya wachezaji wamerejea na kuingia kambini moja kwa moja tangu jana.
"Kocha amewataka wachezaji waingie kambini mapema bila kusubiri waliopo Timu ya Taifa, ana programu za wao pekee kabla ya wale waliopo katika majukumu ya mataifa yao," alisema Bumbuli.