Adhabu aliyopewa msemaji wa Yanga Haji Manara ni mwendelezo wa uthibitisho wa malalamiko ya muda mrefu ya klabu ya Yanga kutotendewa haki na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
Jana Yanga imetoa tamko ikieleza kusikitishwa na adhabu hiyo aliyopewa msemaji wao ambayo wanaamini haiendani na makosa aliyokuwa akituhumiwa nayo kuyafanya
Yanga iko bega kwa bega na Manara ambaye anatarajiwa kukata rufaa kwa mamlaka za juu ya TFF
Manara ametozwa faini ya Tsh Milioni 20 sambamba na kifungo cha miaka miwili kwa makosa ya kudaiwa kumtisha na kumdhalilisha Rais wa TFF, Wallace Karia
Kamati ya Maadili ilitumia uungwana wa Manara kuomba radhi kwa tukio lile lililotokea Arusha kuwa sehemu ya ushahidi wake
Tujikumbushe, kabla ya kutua Yanga Manara alikuwa Afisa Habari wa klabu ya Simba
Wakati yuko Simba kila mmoja anafahamu alifanya makosa makubwa pengine zaidi kuliko hayo aliyotuhumiwa nayo
Lakini kwa kuwa tu kazi yake ilikuwa 'kuinanga' Yanga hakuna aliyejali zaidi malalamiko ambayo Yanga walipeleka TFF dhidi yake, yalipuuzwa
Manara mwenyewe baada ya kutua Yanga alikiri 'aliicharura' kwelikweli Yanga na kuwa haya machungu wanayopitia Simba ni sehemu ndogo sana ya machungu ambayo Yanga wamepitia yeye wakati yuko Simba
Ilikuwa suala la muda tu kwa Manara kufungiwa baada ya kutua Yanga. TFF chini ya uongozi wa Rais Karia ubabe umetumika zaidi kuliko busara, wengi wamefungiwa katika kipindi chake
Tujikumbushe sakata la Morrison; lilishuhudia Afisa habari wa Yanga Hassan Bumbuli na Makamu Mwenyekiti Fredrick Mwakalebela wakifungiwa miaka mitano na kutakiwa kulipa faini ya Tsh Milioni 5 wakati huohuo Manara akiwa msemaji wa Simba na marehemu Zacharia Hans Poppe wakifanya makosa yaleyale, wakatakiwa kulipa faini tu
Adhabu ilikuja kuondolewa baada ya Yanga kukataa rufaa kwenye mamlaka za juu ya TFF
Katika msimu uliopita, Mtendaji Mkuu wa Simba Barbara Gonzalez alimdhalilisha Afisa wa TFF baada ya kumzuia asiingie uwanjani kwenye mchezo kati ya Simba dhidi ya Yanga uliopigwa Disemba 12 2021 katika uwanja wa Benjamin Mkapa
Barbara aliongozana na watoto kadhaa na alitaka kuingia nao kwenye jukwaa la VVIP kinyume na taratibu
Kesi ya udhalilishaji ilifunguliwa Mahakamani lakini busara ilitumika kesi ikafutwa, adhabu aliyopewa Barbara na Kamati ya Maadili ni kulipa faini ya Tsh Laki tano tu!
Kufungiwa kwa Manara kumesherehekewa zaidi na mashabiki wa Simba, wakiamini baada ya Manara kufunguliwa, pengine Yanga itaporomoka
Tuwape pole, hii Yanga ya sasa inapata mafanikio kutokana na uwekezaji mkubwa ambao wadhamini (GSM) waliuweka katika timu
Wiki ijayo Yanga itazindua jezi mpya, Wananchi watavunja rekodi kwa kununua jezi kama wanavyofanya kila msimu
Wananchi watakwenda kujaza uwanja wa Mkapa August 06 kwenye kilele cha wiki ya Mwananchi na August 13 watashuka uwanja wa Mkapa kutetea Ngao ya Jamii dhidi ya Simba
Manara alipojiunga Yanga alifanya kazi sambamba na kina Hassan Bumbuli ambao tayari walikuwa wamefanya kazi nzuri