Aliyekuwa Msemaji wa Yanga Haji Manara amefungua Malalamiko BMT akipinga hukumu Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kumfungia kujihusisha na soka kwa kipindi cha miaka miwili ndani na nje ya nchi pamoja na faini ya Tsh Milioni 20
Akizungumza katika Mkutano na Wanahabari Serena Hotel mapema leo, Manara amesema anapinga hukumu hiyo kwa kuwa kanuni zilizotumika hazikusajiliwa na BMT
Aidha Manara amesema hukumu hiyo ililenga kumdhalilisha na kumzuia asishiriki Tamasha la Wiki ya Mwananchi ambalo kilele chake ni August 06
Manara amesema ameshindwa kukata rufaa kwa kuwa mpaka leo hajapewa nakala ya hukumu, ambayo Kamati ya Maadili ilitangaza kuwa ipo kwa anayeihitaji
Anaamini anacheleweshwa kupata hukumu hiyo ili kuhakikisha wiki ya Mwananchi inapita pamoja na mchezo wa Ngao ya Jamii ili asifanye uhamasishaji
"Hukumu hii pamoja na hukumu zote zilizotolewa na Kamati ya Maadili kwa kutumia kanuni ambazo hazijasaliwa na Baraza la Michezo (BMT) kama sheria za nchi zinavyoelekeza ni BATILI. Nimepeleka malalamiko BMT nikipinga hukumu hii ambayo haijafuata Sheria za nchi"
"Lakini pia hukumu hii ni nuonevu mkubwa kwangu na imelenga kunidhalilisha na kunizuia nisishiriki Wiki ya Mwananchi na klabu ya Yanga. Hakuna matusi ambayo nilimtamkia rais Karia, pale jukwaa kulikuwa na Kamanda wa Polisi, Mkuu wa mkoa wa Arusha, Wakuu wa Wilaya, wabunge na viongozi wengine wa Serikali katika ngazi mbalimbali kama ningefanya makosa hayo naamini wasingeniacha"
"Rais Karia alinifokea pasipo sababu yoyote wakati nikizungumza na Mkuu wa mkoa na hii sio mara ya kwanza kunidhalilisha mbele za watu"
"Siku ile baada ya mchezo, Karia alitamka maneno mabaya ya kuidhalilisha Yanga ambayo kinywa changu hakiwezi kuyatamka. Maneno haya aliyasikia kila mmoja aliyekuwa pale jukwaani (VIP) na ushahidi wake upo," alisema Manara
"Kamati ilininyimwa hata nafasi ya kujitetea kwa kuwa walikataa taarifa halali ya Hospitali ya Temeke ikithibitisha mimi kushindwa kuhudhuria shauri hilo kwa sababu nilikuwa mgonjwa," alisema Manara