Achana na ubabe wa kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi dhidi ya Simba ambapo katika mechi saba za mashindano tofauti walizokutana, ameshinda mara nne, kutoka sare mbili na kupoteza mechi moja
Rekodi hiyo imemfanya Nabi awe kocha wa Yanga aliyeifunga Simba mara nyingi zaidi ndani ya muda mfupi kuliko kocha mwingine yeyote tangu ilipoanzishwa mwaka 1935.
Kocha huyo amedhihirisha umwamba mwingine kwa kuiongoza Yanga kufikia rekodi ya Azam FC ya kucheza mechi 38 mfululizo za Ligi Kuu bila kupoteza baada ya timu yake kupata ushindi wa mabao 2-1 ugenini dhidi ya Polisi Tanzania juzi.
Lakini tofauti na Azam ambayo wakati inaweka rekodi ya kutopoteza mechi 38 ilikuwa chini ya makocha wawili tofauti, Nabi amefikia rekodi hiyo akiiongoza Yanga akiwa pekee ambapo mara ya mwisho kupoteza ilikuwa ni dhidi ya Azam Aprili 25, 2021 walipofungwa bao 1-0.