Katika kuhakikisha kikosi chao kinakuwa imara kuelekea michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika inayotarajia kuanza rasmi kati ya Septemba 9-11, mwaka huu, kikosi cha Yanga kitacheza mechi mbili za kirafiki kabla ya michuano hiyo kuanza, imeelezwa
Moja kati ya timu ambayo Yanga itacheza nayo wakati huu Ligi Kuu Bara ikiwa imesimama kupisha Kalenda ya Fifa, itakuwa dhidi ya AS Arta Solar 7 ya Djibouti, ambayo kikosi chake kinaundwa na baadhi ya nyota wakubwa waliocheza klabu kubwa za Ulaya, wakiwamo Kiungo Mcameroon Alexander Song na winga Solomon Kalou raia wa Ivory Coast.
AS Arta Solar 7, ambao ni mabingwa wa Ligi Kuu Djibouti, wameweka kambi jijini Dar es Salaam kujiandaa na Ligi ya Mabingwa Afrika na katika hatua ya awali ya michuano hiyo itaanzia nyumbani dhidi ya Al-Merrikh ya Sudan.
Kwa mujibu wa Kocha Msaidizi wa Yanga, Cedric Kaze, watakuwa na programu ya mazoezi na mechi za kirafiki kwa kipindi ambacho ligi imesimama kupisha Taifa Stars kucheza mechi za kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN), dhidi ya Uganda.
"Tunarudi katika mazoezi ya gym ili kujiweka sawa kwa kuwa tunaelekea katika michezo migumu, tulipumzika siku mbili na leo tunarudi kazini," alisema Kaze.