Yanga imeanza kujipanga kuelekea msimu mpya wa michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika ambapo mabingwa hao wa soka Tanzania Bara watacheza na Zalan Fc katika hatua ya awali katika michezo ambayo huenda yote ikapigwa jijini Dar es salaam
Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano Rodgers Gumbo amesema wameanza maandalizi yao ambapo tayari wamepokea mahitaji ya benchi la ufundi kuelekea mchezo wa kwanza wa hatua ya awali ambao utapigwa Septemba 09-11 2022
"Tumeshaanza maandalizi kama kamati tuko katika vikao vyetu, tulihitaji mahitaji ya benchi la ufundi ambayo yameshatufikia na baada ya hapo tunaingia msituni kuanza kazi"
"Hizi ni mechi ngumu na kuna umuhimu wa kujua ubora wa wale unaokwenda kukutana nao. Uongozi uko makini sana na unamtafuta mtaalam maalum ambaye ataweza kutupa ubora sahihi wa wapinzani wetu wote tutakaokutana nao lakini pia makocha wetu wakati huu nao wanapambana katika mambo hayo," alisema Gumbo
Kama Yanga itafanikiwa kuvuka hatua ya awali, kwenye raundi ya kwanza itakutana na mshindi wa mchezo kati ya St George ya Ethiopia dhidi ya Al Hilal ya Sudan
Hatua hii ni muhimu zaidi kwani mshindi wa hatua hii atatinga makundi na timu itakayofungwa itapelekwa kwenye michuano ya kombe la Shirikisho kusaka tiketi ya kucheza makundi ya michuano hiyo