Kocha Mkuu wa Yanga Nasreddine Nabi amejijengea heshima ya aina yake kwenye soka la Tanzania
Nabi aliiwezesha Yanga kushinda mataji yote ya ndani msimu uliopita timu hiyo ikiweka rekodi ya kucheza mechi 39 pasipo kupoteza
Yanga waliivunja rekodi ya mechi 38 iliyowekwa na Azam Fc mwaka 2014
Pamoja na furaha ya Wananchi kutokana na mafanikio yaliyoletwa na Nabi, bado wana kiu ya kuiona timu yao ikifanya vizuri Kimataifa
Msimu uliopita Yanga haikufanya vizuri kwenye michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika, ikitolewa kwenye hatua za awali
Msimu huu Yanga inashiriki tena Ligi ya Mabingwa safari hii mchezo wa hatua ya awali watacheza na Zalan Fc mechi zote mbili zikitarajiwa kupigwa uwanja wa Benjamin Mkapa
Akiwa na Yanga, Nabi bado hajashinda mchezo wowote dhidi ya timu kutoka nje ya Tanzania, Wananchi wana shauku kubwa ya kuona timu yao inafanya vizuri Kimataifa kama walivyotawala soka la ndani
Huu ndio mtihani pekee ambao Nabi amebakisha, kuwapa furaha Wananchi kwenye mechi za Kimataifa
Baada ya kuzima tambo za watani zao kwenye soka la ndani, Wananchi wanataka kuona timu yao inafikia na hata kuvuka mafanikio ya watani zao Simba ambao kwa sasa wamebaki kutamba na mafanikio yao kwenye michuano ya CAF