Baada ya kutambulishwa rasmi kuwa Afisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe ameushukuru uongozi wa Yanga chini ya Rais Injinia Hersi Said kwa kumpa nafasi ya kuhudumu katika nafasi hiyo
Aidha Kamwe amewashukuru Wanachama wa Yanga kwa Mabadiliko waliyofanya kwa mfumo wa uendeshaji wa klabu ambayo yamepelekea vijana akiwemo yeye kupata nafasi ya kuhudumu katika klabu ya Yanga
"Kwanza niishukuru Kamati ya Utendaji ya Yanga chini ya Rais Injinia Hersi Said kwa kuniamini na kunipatia nafasi ya kuwa Afisa Habari wa Yanga"
"Lakini pia niwashukuru Wanachama wa Yanga kwani siku ile walipofanya Mabadiliko na baadae kumchagua Injinia Hersi kuwa Rais wa Yanga, ndio mwanzo wa kufunguliwa fursa na sisi vijana kuaminiwa na kupatiwa majukumu haya"
"Wananchi nawapenda sana na nitafanya kazi kwa maarifa makubwa, kwa majaaliwa ya Mwenye ez Mungu tutaweza kufanikisha matarajio ya klabu hii," alisema Kamwe
Kamwe amesema kazi imeanza rasmi na kesho Alhamisi, ataweka hadharani mkakati wa hamasa kuelekea mchezo wa ligi ya mabingwa dhidi ya Al Hilal ambao utapigwa Oktoba 08 katika uwanja wa Benjamin Mkapa
"Hatuwahofii Al Hilal sisi tuna malengo ya kucheza robo fainali ya michuano ya ligi ya mabingwa, hatuwezi kuhofia mechi za hatua ya awali. Kesho tutaweka mkakati wetu kuelekea mchezo dhidi ya Al Hilal. Hawa wachambuzi wasiwatishe, Al Hilal ni timu ndogo sana kwetu," alitamba Kamwe