Baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Ruvu Shooting katika mchezo wa ligi kuu ya NBC uliopigwa uwanja wa Benjamin Mkapa jana, Yanga inahamishia makali yake katika michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika
Jumamosi, Oktoba 08 Wananchi watakuwa katika dimba la Benjamin Mkapa kuwakaribisha Al Hilal kutoka Sudan
Yanga inahitaji kumaliza mchezo huo nyumbani ili kuwa na nafasi ya kutinga hatua ya makundi ambayo walishiriki kwa mara ya mwisho mwaka 1998
Ushindi mnono wa kuanzia mabao mawili au zaidi utaiweka Yanga katika nafasi nzuri ya kusonga mbele
Al Hilal wako DR Congo juzi walicheza mechi ya kirafiki dhidi ya Don Bosco timu inayomilikiwa na ndugu wa Moise Katumbi wa TP Mazembe, wakafungwa mabao 3-1
Tayari mabosi wa Al Hilal wako nchini ambapo jana walikuwepo uwanja wa Benjamin Mkapa kushuhudia mechi ya Yanga. Hata hivyo Jumamosi wasitarajie kuiona Yanga walioishuhudia jana
Wachezaji kama Khalid Aucho aliyecheza kwa dakika chache, Bernard Morrison, Stephane Aziz Ki, Jesus Moloko, Kibwana Shomari wote watakuwepo siku hiyo
Yanga imerejea kambini Avic Town kukamilisha maandalizi ya mchezo huo, ambapo mkufunzi wa timu hiyo Nasreddine Nabi amesema siku tano zitatosha kuwaweka sawa vijana wake