Siku hizi mbili zimekuwa ngumu sana kwa mashabiki wa Yanga kufuatia matokeo ya timu yao dhidi ya Al Hilal katika mchezo wa ligi ya mabingwa mkondo wa kwanza uliopigwa juzi Jumamosi
Wanayanga walikuwa na matumaini makubwa kwa timu yao kupata ushindi katika mchezo huo ambao ulimalizika kwa matokeo ya sare ya bao 1-1
Mwitikio wa mashabiki ulikuwa mkubwa uwanja wa Benjamin Mkapa ambapo Wananchi zaidi ya 45,000 walijitokeza kuishangilia timu yao
Kwa hakika inakatisha tamaa lakini haipaswi kuwa hivyo kwa sababu bado kuna dakika nyingine 90 za kucheza huko Sudan
Matokeo ya mpira wa miguu lazima yaheshimiwe, 'haijamalizika mpaka imalizike' ndio neno ambalo Wananchi wanapaswa kuwa nalo wakielekea mchezo wa marudiano kule Sudan
Sio jambo baya kwa mashabiki kuonyesha hasira zao, viongozi, benchi la ufundi na wachezaji wameona ni kwa kiasi gani wamewaangusha wadau wao muhimu sana siku ya Jumamosi
Sasa wanapaswa kwenda kupigana vita ya kiume huko Sudan ili kuwafuta machozi mashabiki ambao wamechoshwa na kejeli kutoka kwa watani zao
Katika mpira wa miguu hakuna jambo lisilowezekana, naamini Yanga itakwenda Sudan kusaka USHINDI