Kuna uwezekano mkubwa nahodha wa Yanga Bakari Nondo Mwamnyeto akarejea kikosini kwenye mchezo wa marudiano ligi ya mabingwa barani Afrika dhidi ya Al Hilal ambao utapigwa Jumapili Oktoba 16 kunako dimba la Al Hilal huko Sudan
Mwamnyeto alikosa mchezo wa kwanza uliopigwa uwanja wa Benjamin Mkapa mwishoni mwa wiki iliyopita na kumalizika kwa matokeo ya sare ya bao 1-1 lakini ni wazi huduma yake itahitajika huko Sudan
Kutokana na changamoto zilizojitokeza katika eneo la kiungo kwenye mchezo uliopita, Kocha Mkuu wa Yanga Nasreddine Nabi atalazimika kumrudisha Yannick Bangala katika eneo la kiungo wa ukabaji ili katika safu ya ulinzi wa kati akawatumia Dickson Job na Mwamnyeto kama ilivyokuwa msimu uliopita
Yanga inakwenda 'kujilipua' Sudan hivyo ni wazi yapo mabadiliko ya lazima yatafanyika ili kuhakikisha timu inakuwa na uwiano mzuri katika kuzuia na kushambulia tofuati na ilivyokuwa kwenye mchezo uliopita hasa katika dakika 30 za mwisho kwenye kipindi cha pili
Aidha Nabi anaweza kulazimika kuanza na kiungo mshambuliaji mmoja kati ya Feisal Salum na Stephane Aziz Ki ili kukidhi mahitaji ya mfumo wake anaotumia 4-2-3-1
Bangala na Khalidi Aucho ilikuwa pacha bora katika eneo la kiungo msimu uliopita hivyo wawili hao wanafaa kuanza pamoja
Pamoja na kuhitaji kufunga mabao Sudan, Yanga itahitaji kuimarika katika kujilinda kwani ni wazi wenyeji wao Al Hilal nao watahitaji kushinda mbele ya mashabiki wao