Kocha Mkuu wa Yanga Nasreddine Nabi ana siku mbili za kukamilisha maandalizi ya kikosi chake kuelekea mchezo wa kombe la Shirikisho dhidi ya Club Africain ambao utapigwa kesokutwa Jumatano katika uwanja wa Benjamin Mkapa
Ni mchezo muhimu sana kwa Yanga kutumia vyema uwanja wa nyumbani ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kutinga makundi hasa baada ya kuipoteza nafasi ya kucheza makundi ya ligi ya mabingwa
Baada ya Yanga kurejea kutoka Mwanza walikofanikiwa kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Geita Gold na kujikita kileleni mwa msimamo wa ligi, Nabi alisema kikosi chake kina nafasi ya kupata ushindi siku ya Jumatano lakini ni lazima waepuke aina ya makosa waliyofanya kwenye mchezo dhidi ya Al Hilal
"Hii ni mechi ngumu, tunakwenda kukutana na timu ambayo inacheza kwa utamaduni wa Watunisia, kupambana sana kwa nguvu, hii ni lazima tuwe na mabadiliko makubwa katika nidhamu ya ukabaji na kuzuia kwenye eneo letu la ulinzi"
"Najua tunaweza kushinda kwa kuwa tuna ubora wa kutengeneza nafasi na hata kuzitumia, kule mbele tunatakiwa kucheza kwa faida ya timu maombi yangu na nitazungumza sana na wachezaji juu ya umuhimu wa nidhamu ya wakati tumepoteza mpira na wakati tunao," alisema Nabi
Club Africain hawana historia kubwa kwenye michuano ya kombe la Shirikisho katika misimu ya karibuni licha ya kuwa moja ya klabu kongwe huko Tunisia
Ni timu ambayo haina rekodi nzuri katika mechi zao za ugenini kwenye michuano ya CAF, wanakuwa bora zaidi wanapokuwa nyumbani
Yanga inapaswa kumaliza mchezo siku ya Jumatano ili kwenda Tunisia kwa lengo la kwenda kusaka sare tu