Sare tasa dhidi ya Club Africain ni matokeo ambayo Wananchi hawakuyatarajia. Utaona ni kama mashabiki wa Yanga sasa wamekata tamaa na timu yao wakiamini haiwezekani kwenda kupata ushindi ugenini
Wakati mwingine mpira una matokeo ya kikatili sana, ndivyo ilivyo. Wengi watalalamika, watalaumu na hata kutukana ni kwa sababu hawakufurahishwa na matokeo
Baada ya Yanga kuondoshwa kwenye michuano ya ligi ya mabingwa na Al Hilal, matumaini ya Wananchi ilikuwa kuona timu yao ikifanya vizuri kwenye mchezo dhidi ya Club Africain
Sasa wanaona hakuna hatua yoyote iliyopigwa kutoka mchezo dhidi ya Al Hilal na huu dhidi ya Club Africain
Matokeo haya yameumiza kila Mwanayanga. Wanachama, mashabiki, viongozi, benchi la ufundi na hata wachezaji
Wachezaji wanajua wamewaangusha mashabiki wao ambao wamekuwa wakijitoa kuwaunga mkono. Matokeo haya yameshusha morali ya mashabiki na haitashangaza kuona idadi ya wale wanaokwenda uwanjani inapungua
Kuna dakika nyingine 90 muhimu kule Tunisia. Kiuhalisia bado mchezo huu uko 50-50 kwani yeyote atakayeshinda mchezo wa pili atasonga mbele
Hakuna jambo lisilowezekana kwenye mpira wa miguu, wanachopaswa kufanya Yanga huko Tunisia ni kufunga bao/mabao
Bao moja la Yanga litakuwa na thamani ya mabao mawili ya Club Africain, mabao mawili ya Yanga yatakuwa na thamani ya mabao matatu ya Club Africain na idadi itaongezeka kwa mtiririko huo
Utaona ni kwa kiasi gani hata Club Africain wenyewe watakuwa na wakati mgumu kuikabili Yanga, ili kuweza kuifunga Yanga watahitaji kufunguka na wakifanya hivyo hata Yanga itakuwa na nafasi
Jana Club Africain waliweka watu tisa nyuma ya mpira, hawakutaka mpira uchezwe kabisa lakini huko kwao hawatafanya hivyo kwani watahitaji kufunga kwa sababu matokeo yakiisha 0-0 mikwaju ya penati itaamua mshindi
Sasa hii ni Yanga sio Kipanga, huko kwao Club Africain hawatapata uhuru walioupata walipocheza na Kipanga na kushinda mabao 7-0
Mwaka 2017 katika hatua ya nusu fainali michuano hii Club Africain walicheza na Super Sport United ya Afrika Kusini, mchezo wa kwanza ulipigwa Afrika Kusini, ulimalizika kwa sare ya bao 1-1
Super Sport United wakashinda mabao 3-1 katika mchezo wa marudiano uliopigwa Tunisia
Binafsi nitakuwa mtu wa mwisho kuamini Yanga tayari imendoshwa katika mashindano, nitaamini hilo baada ya dakika 90 za Tunisia