Benchi la ufundi na wachezaji wa Yanga wanafahamu umuhimu wa mchezo dhidi ya Club Africain ambao utapigwa Jumatano, Novemba 09 huko Tunisia
Uwekezaji mkubwa uliofanywa na GSM, unawapa kila sababu Yanga kucheza makundi ya kombe la Shirikisho baada ya kukosa nafasi hiyo kwenye michuano ya ligi ya mabingwa
Kwa ligi ya ndani Yanga imejihakikishia utawala wa aina yake, lakini pamoja na mafanikio hayo Yanga itaonekana si lolote wala chochote kama itaondoshwa na Club Africain
Kejeli, matusi, kashfa na dharau kwa Wananchi zimetamalaki kila kona baada ya matokeo ya mchezo wa kwanza dhidi ya Club Africain uliopigwa uwanja wa Benjamin Mkapa na kumalizika kwa suluhu ya bila kufungana
Ukiangalia nyuso za wachezaji wa Yanga, unaona kabisa wamedhamiria kufanya jambo siku ya Jumatano
Kwa kocha Nasreddine Nabi huu ni mchezo muhimu sana kwake. Ni kocha aliyeirejesha heshima ya Yanga iliyopotea misimu minne iliyopita
Lakini huko vijiweni wanamsema kuwa yeye uwezo wake ni wa ndani tu, Kimataifa amefeli
Wasichofahamu hao wanaombeza, Nabi amewahi kutwaa taji hili la michuano hii mwaka 2012 akiwa na AC Leopards ya Congo
Ni michuano ambayo si migeni kwake na anafahamu aina ya presha atakayokutana nayo kama Yanga itashindwa kupata ushindi dhidi ya Club Africain
Ukiangalia mwendendo wa mchezo wa kwanza, jambo pakee ambalo unaweza kusema Club Africain walifanikiwa ni kufanya mpira usichezwe
Ulikuwa mpango mkakati wao kuhakikisha Yanga hawapati utulivu katika mpira wakitumia kila aina ya mbinu kumhadaa mwamuzi kwa kujiangusha au kuchelewesha matukio
Naamini mchezo wa Jumatano hawatafanya hivyo, watacheza kusaka bao la mapema
Huu ndio mtego pekee ambao Yanga itahitaji kuutegua, kuwa makini kutowaruhusu kupata bao mapema na zaidi kama Yanga itatangulia kufunga basi mchezo utakuwa wazi
Katika mechi nne za mwisho ambazo Club Africain wamecheza nyumbani katika michuano ya CAF, wameshinda mbili na kupoteza mbili
Kabla ya ushindi wa mabao 7-0 dhidi ya Kipanga, walifungwa mechi mbili dhidi ya Super Sport United na RS Berkane