Kocha Mkuu wa Yanga Nasreddine Nabi leo anahitaji kuchanga karata zake vyema katika mchezo wa mkondo wa pili mtoano kombe la Shirikisho dhidi ya Club Africain
Mchezo huo ambao utaamua timu inayokwenda hatua ya makundi ya michuano hiyo, utapigwa saa 2 usiku kwa saa za Tanzania
Baada ya kulazimishwa matokeo ya suluhu ya bila kufungana katika mchezo wa mkondo wa kwanza, leo Yanga inahitaji kushinda au hata matokeo ya sare ya mabao, yatatosha kuwapeleka Wananchi makundi
Habari njema kwa Nabi ni kuwa wachezaji wake wote wako tayari kwa mchezo huo
Salum Abubakar 'Sureboy' alikuwa kwenye hatihati ya kukosekana lakini baada ya kufanya mazoezi na wenzake kwa siku tatu, Afisa Habari wa Yanga Ali Kamwe amethibitisha yuko fiti kuwakabili Club Africain
Mchezo wa leo unatarajiwa kuwa tofauti na mchezo wa mkondo wa kwanza ambao Club Africain hawakufunguka. Leo wako nyumbani mbele ya mashabiki wao, ni wazi watajaribu kushambulia hasa kutafuta bao la mapema
Nabi anatarajiwa kuweka uimara kwenye safu ya ulinzi lakini pia kushambulia kwa haraka na pale watakapopata nafasi wazitumie kwani inawezekana mchezo wa leo usiwe na nafasi nyingi
Kukosekana kwa Djuma Shabani ambaye alibaki jijini Dar es salaam akiwa majeruhi, huenda Nabi akamtumia Dickson Job kwenye safu ya ulinzi upande wa kulia wakati Kibwana Shomari akiendelea kutumika upande wa kushoto
Nahodha Bakari Nondo Mwamnyeto leo anaweza kurejeshwa kikosini kucheza sambamba na Yannick Bangala katika eneo la ulinzi wa kati
Lakini pia Nabi anaweza kumtumia Kibwana upande wa kulia na kushoto akamtumia Farid Mussa au Joyce Lomalisa ili Job na Bangala wakaendelea kutumika eneo la ulinzi wa kati
Feisal Salum 'Fei Toto' huenda leo akacheza namba 10 na pengine Stephane Aziz Ki akahamishiwa winga wa kulia na hivyo eneo la kiungo wanaweza kushuhudiwa Khalid Aucho na Salum Abubakar au Gael Bigirimana wakianza
Benard Morrison na Fiston Mayele wanatarajiwa kuendeleza pale walipoishia kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza uliopigwa jijini Dar es salaam wiki iliyopita
Mchezo wa leo ni kama fainali kwani mshindi lazima apatikane. Kama mchezo utamalizika kwa suluhu ya bila kufungana, kutakuwa na changamoto ya mikwaju ya penati
Wachezaji wa Yanga wanapaswa kuhakikisha hawapotezi mchezo ndani ya dakika 90, matokeo mengine yoyote yanaweza kuwa na faida kwao
Ikishindikana kabisa kushinda ni bora kwenda kwenye mikwaju ya penati, Djigui Diarra amekuwana rekodi nzuri sana inapokuja changamoto ya mikwaju ya penati