Kocha Mkuu wa Yanga Nasreddine Nabi amesema mshambuliaji Clement Mzize atapata mafanikio makubwa kama ataendelea kujituma na kufuata maelekezo ya walimu wake
Mzize alifunga bao pekee la Yanga kwenye mchezo wa ligi kuu dhidi ya Kagera Sugar uliopigwa uwanja wa CCM Kirumba
Nabi alilazimika kumtumia Mzize katika mchezo huo ili kuwapa mapumziko baadhi ya wachezaji ambao walitoka kucheza mechi mfululizo
Pengine huo ukawa mwanzo wake mpya katika kikosi cha kwanza kwani alionyesha yuko tayari kwa majukumu ya timu ya wakubwa
Nabi amemsifia kinda huyo kuwa ni mpambanaji na anamuona akipata mafanikio makubwa kwenye soka la tanzania
"Mzize ni mchezaji mzuri mpambanaji na sahihi kwenye eneo analocheza kutokana na umbo lake na mikimbio yake uwanjani namuona mbali atakuja kuwa staa wa Tanzania eneo la ushambuliaji kama ataendeleza ubora wake alioanza nao," alisema Nabi
Baada ya kumuona anafanya vizuri kwenye timu ya vijana, Nabi alipendekeza kinda huyo mwenye umri wa miaka 18 apandishwe timu ya wakubwa
Nabi ameahidi kuendelea kumtumia kulingana na mahitaji ya timu na pengine anaweza kumjumuisha kwenye kikosi kitakachoshiriki hatua ya makundi kombe la Shirikisho