Afisa Habari wa Yanga Ali Kamwe amesema kuelekea mchezo wa ligi kuu dhidi ya Mbeya City ambao utapigwa uwanja wa Benjamin Mkapa, hawatakuwa na utaratibu wa kusimama kwenye dakika ya 48
Tukio la pongezi kwa wachezaji na benchi la ufundi litafanyika baada ya mchezo kumalizika, ambapo kutakuwa na shamrashamra kufurahia rekodi kubwa ambayo Yanga wanaweza kuweka
Yanga imecheza mechi 48 pasipo kupoteza mchezo kwenye ligi, kama haitapoteza mchezo dhidi ya Mbeya City, basi itafikisha mechi 49 na kufikia rekodi iliyowahi kuwekwa na Arsenal kule Uingereza msimu wa 2003/04
"Kesho tunawania rekodi kubwa ya kucheza mechi 49 pasipo kupoteza. Sio jambo dogo kufikia rekodi hiyo, tumeandaa utaratibu tofauti wa kushangilia"
"Hatutasimama kwenye dakika ya 48 kwa kufuata utaratibu wa mechi zilizopita, bali shamrashamra tutazifanya baada ya mchezo kumalizika"
"Tunaweza kufikia rekodi iliyowahi kuwekwa na Arsenal, tumewaalika mashabiki wa Arsenal waje waungane nasi katika shamrashamra za kucheza mechi 49," alitamba Kamwe
Kamwe amesema wataingia kwenye mchezo huo wakiiheshimu Mbeya City kama walivyofanya katika timu nyingine walizokutana nazo lakini anaamini ubora wa kikosi chao unawapa sababu ya kushinda mchezo huo
"Sisi katika mechi 11 za ligi, tumeshinda mechi tisa, Mbeya City katika mechi 13 wameshinda nne, tunawaheshimu lakini sisi tuko katika daraja tofauti na tumedhamiria kuendeleza rekodi yetu nzuri"