Yanga imerejea mazoezini kujiandaa na mchezo wa ligi kuu dhidi ya Tanzania Prisons ambao utapigwa Jumapili, Disemba 04 katika uwanja wa Benjamin Mkapa
Baada ya kupoteza mchezo uliopita dhidi ya Ihefu Fc, hii ni nafasi kwa wachezaji wa Yanga kuwadhihirishia mashabiki wao kuwa walipoteza mchezo uliopita kwa bahati mbaya, dhamira yao ya kutetea ubingwa kwa msimu wa pili mfululizo iko palepale
Wanakwenda kuikabili Tanzania Prisons ambayo katika misimu ya karibuni imekuwa ikiisumbua Yanga katika mechi zilizopigwa uwanja wa Mkapa
Msimu uliopita Prisons walifanikiwa kuondoka na alama moja mbele ya Yanga katika mchezo uliomalizika kwa matokeo ya suluhu ya bila kufungana
Walifanya hivyo pia katika msimu mwingine nyuma katika mchezo uliomalizika kwa matokeo ya sare ya bao 1-1
Wadhamini wa Tanzania Prisons, Silent Ocean wameiahidi kitita cha Tsh Milioni 20 kama wataifunga Yanga, Milioni 10 kama watatoka sare dhidi ya Yanga
Hata hivyo hii ni mechi muhimu sana kwa Yanga, wachezaji wanaitaka kwelikweli ili kunyamazisha kelele za watani zao
Ushindi kwa Yanga kwenye mchezo huo utawahakikishia kumaliza mechi za duru ya kwanza wakiwa kileleni mwa msimamo wa ligi kabla ya mechi yao ya kiporo dhidi ya Namungo Fc itakayopigwa Disemba 07, Ruangwa