Kocha Msaidizi wa Yanga Cedric Kaze amesema wananchi watarajie kuona Yanga tofauti kabisa na ile waliyoishuhudia kwenye mchezo wa ligi kuu dhidi ya Ihefu Fc
Kesho Jumapili Yanga itashuka uwanja wa Benjamin Mkapa kuikabili Tanzania Prisons katika mchezo wa ligi kuu ya NBC
Akizungumza katika Mkutano na Wanahabari mapema leo, Kaze alisema wamekamilisha maandalizi kuelekea mchezo huo licha ya kuwa watawakosa baadhi ya wachezaji kutokana na sababu mbalimbali
"Tutamkosa Dickson Job anatumikia adhabu ya kadi tatu za njano, Fiston Mayele na Jesus Moloko hawakufanya mazoezi na timu kwa siku kadhaa kutokana na majeraha lakini tutaangalia utayari wao katika mazoezi ya mwisho leo. Nahodha Bakari Mwamnyeto nae bado hayuko sawa"
"Lakini tunafurahi kuona baadhi ya wachezaji wamerejea Farid Mussa, Djuma Shaban, Benard Morrison hayuko sawa kwa asilimia 100 lakini amerejea"
"Tutakuwa na mabadiliko madogo kwenye kikosi chetu lakini muhimu mtashuhudia Yanga tofauti kabisa na ile mliyoiona ikicheza na Ihefu Fc," alisema Kaze
Katika hatua nyingine, Kaze ameishauri Bodi ya Ligi kupanga ratiba ambayo ni rafiki kwa timu zote
Amesema baadhi ya mechi zinakosa ubora na hadhi ya ligi kuu kutokana na changamoto ya ratiba ngumu
"Kuna timu zinasafiri kwa basi hadi kilomita 800 halafu wanapaswa kucheza mechi kila baada ya siku tatu, hii ni ratiba ngumu sana"
"Mfano sisi tunacheza na Prisons Jumapili baada ya mechi hiyo, usiku tutaondoka kuelekea Mtwara na kisha kuunganisha Lindi takribani kilomita 200 tunakabiliwa na mchezo dhidi ya Namungo Fc Disemba 07"