Wananchi wametakata uwanja wa Majaliwa mkoani Lindi wakiibuka na ushindi wa mabao 2-0 katika mchezo wa ligi kuu dhidi ya Namungo Fc
Ulikuwa mchezo wa kufunga mechi 15 za duru ya kwanza, Yanga ikifanikiwa kuongeza alama tatu na kuzidi kujichimbia kileleni mwa msimamo wa ligi
Yannick Bangala aliitanguliza Yanga kwenye dakika ya 40 akimalizia mpira uliotemwa na mlinda lango wa Namungo Fc Jonathan Nahimana baada ya shuti la adhabu kutoka kwa Stephane Aziz Ki
Yanga ilikwenda mapumziko ikiwa inaongoza bao 1-0
Wananchi wakarejea kipindi cha pili wakiwa na kasi ileile licha ya Namungo kujaribu kusaka bao la kusawazisha
Hata hivyo alikuwa Tuisila Kisinda aliyepigilia msumari wa mwisho kwenye jeneza la Namungo katika dakika ya 83 baada ya kufunga bao safi akiwatoka walinzi wa Namungo kabla ya kuuweka mpira kimiani
Yanga imejichimbia kileleni mwa msimamo wa ligi baada ya kufikisha alama 38




