Siku chache baada ya kupewa mkataba wa kuiongoza timu ya wanawake ya Yanga Princess iliyopo Ligi Kuu (WPL), Sebastian Nkoma amesema amekubali kuingia makubaliano ya kuinoa timu hiyo baada ya kubaini ina kikosi kizuri na bora ambacho anaweza kukiongoza kutwaa ubingwa
Nkoma aliyewahi kuwa mkufunzi wa Simba Queens, amesema ameingia katika timu hiyo akiwa na maswali mawili ya kujiuliza ikiwa ni pamoja na kwanini timu hiyo imeshindwa kutwaa taji ndani ya misimu minne mfululizo kwani alikuwa akiifuatilia kabla na kutamba chini yake anaamini itawezekana kwa vile ina kikosi bora.

"Ni mapema sana kuzungumza moja kwa moja nimetua kuleta taji nahitaji kukaa na timu kwa kuiongoza hata michezo mitano ili niangalie mapungufu na ubora ulipo ili niweze kuongeza nguvu yangu," Nkoma alinukuliwa na gazeti la Mwanaspoti
"Kuna baadhi ya wachezaji wapo nimefanya nao kazi nilipokuwa Simba kina Maimuna na sikumaliza nao vibaya ni rahisi kwangu kuanza kufanya nao kazi vizuri pia kuna wengine nimekutana nao timu ya Taifa, nahitaji kuona wanaendeleza nidhamu na ushindani ili tuweze kufikia malengo"
"Nimeona usajili mzuri na naamini dhamila ya uongozi ni kuona timu inapata mafanikio. Natamani kuthibitisha usajili uliofanywa kwa kuchanganya wachezaji kutoka mataifa mbalimbali kama unaendana na mahitaji na kama sivyo walivyokuwa wanatarajia nitakuwa na kitu cha kuwaeleza ili tujue wapi tunaboresha zaidi na wapi tumekosea"
Mchezo wa wake wa kwanza ni kesho dhidi ya Mkwawa Queens ambao utapigwa uwanja wa Uhuru