Baada ya shamrashamra za sikukuu ya Christmas, usiku majira ya saa mbili na robo, Yanga itakuwa uwanja wa Benjamin Mkapa kuwakabili wauza Ice Cream, Azam Fc katika mchezo wa ligi kuu ya NBC unaotarajiwa kuwa na upinzani mkali
Baada ya mjadala kuhusu mkataba wa Feisal Salum kuhitimishwa hapo jana, sasa ni muda wa kuonyeshana kazi uwanjani
Jambo pekee ambalo Azam Fc wamefanikiwa mpaka sasa ni kumuondoa Fei Toto katika mchezo huo na kuwanyima fursa Wananchi na Watanzania kumshuhudia kiungo huyo mahiri leo
Yawezekana ulikuwa mpango mkakati wao kuhakikisha Fei hashiriki mchezo huo wakikumbuka ndiye aliyefunga mabao yote mawili katika mchezo wa kwanza uliomalizika kwa matokeo ya sare ya mabao 2-2
Hata hivyo Yanga hii ya Kocha Nasreddine Nabi haitegemei mchezaji mmoja, imedhihirisha hilo katika mechi nyingi walizocheza msimu huu bila ya wachezaji wake muhimu na kufanikiwa kupata ushindi
Ni mechi inayotarajiwa kuwa na upinzani mkali hasa baada ya jaribio walilofanya Azam Fc, ni kama wametangaza vita dhidi ya Yanga
Leo Yanga itaingia katika mchezo huo ikiwa kwenye kiwango bora sana kulinganisha na mechi ya kwanza
Tangu walipopoteza dhidi ya Ihefu Fc, Wananchi wamecheza na kushinda mechi tano mfululizo
Katika mechi hizo hawakuruhusu bao kutikisa nyavu zao huku mechi mbili za mwisho Coastal Union na Polisi Tanzania wakishindwa hata kupiga 'shoot on target'
Azam Fc watarajie kukutana na 'suprise' ya aina yake kutoka kwa vijana wa Nabi ambao dhamira yao ni kushinda mchezo huo ili kuongeza gap la pointi dhidi ya Azam Fc kutoka saba na kufikia 10