Stephane Aziz Ki leo atakuwa mchezaji muhimu kwenye kikosi cha Yanga katika mchezo wa ligi kuu dhidi ya Azam Fc ambao utapigwa uwanja wa Benjamin Mkapa
Baada ya sintofahamu iliyojitokeza kuhusu Feisal Salum 'Fei Toto', ni wazi Aziz Ki leo atasimamia mashambulizi ya Yanga akitokea eneo la kiungo katika mchezo ambao Yanga inahitaji kushinda
Pengine Yanga leo itakuwa hatari zaidi kwani Kocha Nasreddine Nabi atamtumia kila mchezaji katika eneo sahihi
Kukosekana kwa Fei Toto kunamaanisha Salum Abubakar 'Sure Boy' huenda akaanza sambamba na Khalid Aucho katika eneo la kiungo huku Aziz Ki akicheza mbele yao
Katika mchezo wa ligi uliopita dhidi ya Coastal Union, Aziz Ki alihusika katika mabao yote matatu yaliyofungwa na Yanga. Alitoa pasi za mabao mawili na kuanzisha shambulizi la bao jingine moja
Upo mjadala ambao uliibuliwa na wachambuzi walioamini kuwa Feisal anapaswa kutumika katika nafasi ya Aziz Ki kwani amekuwa na ufanisi zaidi anaporikaribia goli
Zipo nyakati Nabi alimtumia Aziz Ki eneo la winga na wakati mwingine kumuacha nje ili Feisal acheze namba 10
Yawezekana bado hajafikia kile kiwango alichokuwa nacho Asec Mimosas, lakini hilo halifuti ukweli Aziz Ki ni mchezaji hatari na aliyekamilika zaidi
Ni mchezaji mwenye maamuzi sahihi, anafahamu ni wakati gani apige shuti au atoe pasi kwa wenzie. Angalia mipira yake ya faulo inavyozalisha mabao kwa Yanga
Ukizungumzia mchezaji aliyehusika katika mabao mengi ya Yanga kwenye mechi tano zilizopita, ni Aziz Ki
Wachezaji wanafuatilia mijadala na kila kinachoendelea mitandaoni, Aziz Ki anafahamu leo ni siku muhimu kwake kuwapa majibu wale wenye mashaka nae
Miguu ya Aziz Ki leo inaweza kuzima au kukoleza mjadala kuhusu nafasi ya Feisal kwenye kikosi cha Yanga