Jana Azam Fc walikuwa wenyeji wa mchezo dhidi ya Yanga uliopigwa uwanja wa Benjamin Mkapa na Wananchi kuibuka na ushindi wa mabao 3-2
Kwa kawaida Azam Fc katika mechi zao ambazo wako nyumbani hutumia jezi zenye rangi ya blue, hata hivyo jana wakabadili na kutumia nyeusi ili kuizuia Yanga kutumia jezi zao nyeusi ambazo wamezitumia zaidi katika mechi walizocheza hivi karibuni
Wakiwa na imani kwamba kama Yanga haitavaa jezi nyeusi basi wataweza kuifunga; mambo hayakuwa hivyo
Wananchi wakatumia uzi wao wa kijani na wakaondoka na alama zote tatu
Ilikuwa mechi ambayo ilitawaliwa na propaganda nyingi nje ya uwanja ikiwa ni pamoja na kuhakikisha Yanga haimtumii kiungo wake Feisal Salum 'Fei Toto' ambaye aliondoka kambini siku ya Ijumaa na kuzima simu zake huku akiandika barua ya kuvunja mkataba wake
Bahati mbaya jaribio hilo halikuzingatia matakwa ya kisheria hivyo Azam Fc watalazimika kufika mezani kujadiliana na Yanga kama wanamuhitaji Feisal
Baada ya kipigo hicho, matumaini pekee yaliyobaki kwa Azam Fc ni kupambana na Simba katika nafasi ya pili kwani watahitaji muujiza kuwa mabingwa msimu huu