Kikosi cha Yanga kiko tayari kwa mchezo wa ligi kuu dhidi ya Ihefu Fc ambao utapigwa kesho Jumatatu, Januari 16 katika uwanja wa Benjamin Mkapa
Akizungumza katika Mkutano na Wanahabari kuelekea mchezo huo, Kocha Msaidizi wa Yanga Cedric Kaze amesema wamejiandaa vyema kuikabili Ihefu Fc katika mchezo ambao anaamini utakuwa mgumu
"Sisi tuko tayari kwa mchezo, tunafahamu hautakuwa mchezo rahisi kwa sababu Ihefu Fc wana timu nzuri na wamefanya maboresho katika dirisha hili la usajili"
"Lakini naamini tuko katika wakati mzuri zaidi kucheza nao kuliko vile tulivyokutana katika mchezo wa kwanza ambao walitufunga," alisema Kaze
Aidha Kaze amesema baadhi ya wachezaji watakosa mchezo huo kutokana na sababu mbalimbali
"Zawadi Mauya aliumia kwenye michuano ya kombe la Mapinduzi wakati Aboutwalib Mshery alirejea mazoezini lakini ameumia tena. Pia tutawakosa Yannick Bangala, Bernard Morrison na Stephane Aziz Ki"