Leo Yanga inakwenda kuikabili Ruvu Shooting ikiwa katika wakati mzuri sana, matumaini ni makubwa kwa Wananchi kuendeleza ubabe wao katika ligi kuu ya NBC
Baada ya ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya Ihefu Fc, kikosi cha Yanga kimepata wiki moja ya kufanya maandalizi ya kuikabili Ruvu Shooting
Habari njema zaidi ni kurejea kikosini kwa wachezaji ambao walikosekana katika mchezo uliopita na kuibua malalamiko kutoka kwa mashabiki dhidi ya uongozi wao kuhusu ruhusa za wachezaji wakati ligi ikiwa inaendelea
Winga mtukutu Bernard Morrison anaweza kuwa miongoni mwa wachezaji ambao watashuka dimbani leo
Morrison amekuwa na takribani siku tano za kufanya mazoezi na wachezaji wenzake tangu aliporejea kutoka Ghana
Nyota wengine ambao wanaweza kurejea kikosini leo ni Stephane Aziz Ki na Yannick Bangala wakati beki mpya Mamadou Doumbia anaweza kupata dakika chache katika mchezo huo kama sehemu ya utambulisho
Mashabiki wa Yanga wanasubiri kuona ni namna gani kocha Nasreddine Nabi leo atawatumia washambuliaji Fiston Mayele na Kennedy Musonda ambao katika mchezo uliopita dhidi ya Ihefu Fc walikuwa hatari katika dakika 27 walizocheza pamoja
Yanga inahitaji kushinda leo ili kuzidi kusogelea ubingwa wa 29 ligi kuu, hesabu ya kushinda mechi nane inaanza leo