Msemaji wa zamani wa Yanga Haji Manara ametamba kuwa Wananchi wanaweza kutangaza ubingwa wa ligi kuu kabla ya sikukuu ya Pasaka
Manara ambaye anatumikia adhabu ya kufungiwa miaka miwili na faini ya Tsh Milioni 10, amesema ubora wa kikosi cha Yanga kulinganisha na wapinzani wake kwenye ligi, unawapa kila sababu ya kuamini watatwaa ubingwa kwa msimu wa pili mfululizo
"Kama mnakumbuka vyema mwaka jana niliachia takwimu kwa nini Yanga itashinda ubingwa na nikaweka sababu ambazo huwa zinashinda porojo"
"Msimu huu ukiacha Takwimu bora tulizonazo, lakini kubwa Yanga ina wachezaji bora ambao timu nyingi hawana katika Premier league"
"Tukiwa tumemaliza theluthi mbili ya mechi zote na huku tukionyesha ubora ambao huwa hauzidiwi na lolote isipokuwa bahati, YANGA Afrikaaaaaaa inawezekana kushinda Ubingwa huu kabla ya Sikukuu za Pasaka na mechi yetu na Madunduka ikawa ni kukamilisha ratiba, sanasana watupigie Guard of Honor," alitamba Manara
Kimahesabu, kama Yanga itashinda mechi zote saba zinazofuata, basi itajihakikishia ubingwa wa 29
Ni timu moja tu (Simba) ambayo inaonekana kubaki kwenye mbio za ubingwa ikiwa nyuma kwa tofauti ya alama sita dhidi ya Yanga
Simba inakabiliwa na mechi mbili muhimu (dhidi ya Azam na Singida Big Stars) ambazo nazo zina vita yao kuwania nafasi ya kushiriki michuano ya CAF msimu ujao
Azam Fc na Singida BS zote zina alama 43 katika nafasi ya tatu na nne Azam Fc ikiwa juu kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa. Ziko nyuma ya Simba inayoshika nafasi ya pili kwa tofauti ya alama saba
Mchezo unaofuata kwa Simba kwenye ligi ni dhidi ya Singida Big Stars na kisha kufuatiwa na mchezo dhidi ya Azam Fc huku Yanga ikicheza dhidi ya Namungo Fc na kufuatiwa na mchezo dhidi ya KMC