Juzi kiungo Gael Bigirimana aliondoka nchini ikielezwa kuwa amefikia makubaliano ya kuvunja mkataba wake wa mwaka mmoja na nusu na klabu ya Yanga
Bigirimana alijiunga na Yanga kwenye dirisha la usajili la Julai 2022 akisaini mkataba wa miaka miwili
Kwa kuangalia CV yake, akiwa amecheza ligi kuu ya Uingereza klabu ya Newcastle United pia kuitumikia timu ya Taifa ya U20 ya Uingereza, kulikuwa na matumaini mkubwa kwa Bigirimana kufanikiwa katika kikosi cha Yanga, lakini haikuwa hivyo
Katika dirisha dogo la usajili, Yanga ilihitaji nafasi mbili za wachezaji wa kigeni kwa ajili ya maboresho ya kikosi, ikalazimika kuchukua maamuzi magumu kwa kuwaondoa Heritier Makambo na Bigirimana huku nafasi zao kuchukuliwa na Kennedy Musonda na Mamadou Doumbia
Katika eneo la kiungo Yanga pia ikamuongeza mzawa Mudathir Yahya ambaye kiuhalisia ndiye aliyechukua nafasi ya Bigirimana
Mudathir ameongeza ubora katika kiungo cha Yanga pengine kuliko hata alivyofanya Bigirimana
Wakati mwingine usajili ni kamali, mchezaji anaweza kufanikiwa timu moja na kushindwa katika timu nyingine
Ndivyo ilivyokuwa kwa Bigirimana ambaye pia hucheza timu ya Taifa ya Burundi