Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya michezo nchini, Ally Mayay amewashauri wachezaji wa Kitanzania kuwa na Mameneja ambao watawasimamia mambo yao ikiwemo suala la mikataba ili kuepuka migogoro
Mayay ametoa kauli hiyo kufuatia sintofahamu ya mkataba iliyojitokeza kati ya kiungo Feisal Salum na klabu ya Yanga
Aidha, Mayay amezitaka pande zote zinazohusika kwenye sakata hilo kukaa mezani kulimaliza ili kila upande uweze kunufaika
"Moja ya mapungufu ambayo tumeyaona ni wachezaji kutokuwa na mameneja ambao wanawasimamia, suala la kuwa na meneja kwa sasa hakukwepeki"
"Wote ni wadau wa michezo tunataka mafanikio kwa hiyo tunaomba masuala haya yamalizwe, pande zote mbili ziwe zimekubaliana kwa sababu sisi Serikali ni wazazi tunataka mafaniko ya wote," Mayay alinukuliwa na gazeti la Mwananchi
Baada ya Feisal kutangaza kuvunja mkataba wake, klabu ya Yanga ilipinga kwa kufungua shauri Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shiririkisho la Mpira wa mIguu Tanzania (TFF)
Kamati hiyo ikathibitisha Mkataba wa Feisal na Yanga ni halali kwa kuwa mchezaji huyo hakufuata taratibu za kuuvunja
Hata hivyo tangu Kamati itoe hukumu, Feisal bado hajarejea kwenye kikosi cha Yanga ambapo mapema wiki hii Mtendaji Mkuu wa Yanga Andre Mtine alimuandikia barua kumtaka arejee kuendelea na majukumu yake kama mkataba unavyomuelekeza
Licha ya Feisal 'kutokomea kusikojulikana', Yanga imeendelea kutimiza wajibu wake kwa kumlipa mshahara na bonus kwa mujibu wa makubaliano ya mkataba
Kama jambo hili halipatiwa ufumbuzi ni wazi Feisal ataendelea kuwa nje ya uwanja pengine mpaka mkataba wake utakapomalizika mwezi Juni 2024, zaidi anaweza kukumbana na adhabu kubwa zaidi kutoka mamlaka za usimamizi wa soka kama Yanga itaamua kumchukulia hatua kwa 'utoro'