Siku ya Jumapili Wananchi watafurika uwanja wa Benjamin Mkapa katika mchezo wa hatua ya makundi kombe la Shirikisho dhidi ya TP Mazembe. Mchezo huo utapigwa saa 1 usiku
Ni mechi ambayo inakuja na matukio na kumbukumbu tofauti kwa mashabiki wa Yanga
Kwanza ni kurejea kwa aliyekuwa kiungo wao pendwa Mukoko Tonombe ambaye alijiunga na TP Mazembe katika dirisha dogo la usajili msimu uliopita
Mukoko aliitumikia Yanga kwa mwaka mmoja na nusu akiwa mmoja wa wachezaji waandamizi
Hata hivyo baada ya usajili mkubwa uliofanywa na Yanga kuelekea msimu wa 2021/22, Mukoko alikumbana na wakati mgumu kupata nafasi kwenye kikosi cha kocha Nasreddine Nabi
Baadae Yanga iliamua kumtumia katika makubaliano ya usajili wa winga Chico Ushindi aliyetoka Mazembe kuja Yanga na Mukoko kujiunga na Mazembe
Jumapili itakuwa mara ya kwanza kwa Mukoko kukutana na waajiri wake hao wa zamani
Lakini pia hii ni mechi ya kisasi kwa Yanga, timu hizi zilikutana kwenye michuano hii mwaka 2016 wakati huo hatua ya makundi ikiwa na timu nane tu Yanga ikipangwa kundi A na timu za TP Mazembe, Mo Bejaia na Medeama

TP Mazembe waliibuka na ushindi wa bao 1-0 katika mchezo ambao uliibua kipaji cha winga Juma Mahadhi ambaye hata hivyo majeraha yaliathiri muendelezo wa kipaji chake
Wananchi wanakumbuka katika mchezo huo, aliyekuwa Mwenyekiti wakati huo Yusufu Manji aliwalipia mashabiki wote viingilio na hivyo uwanja wa Mkapa kujaa ilipofika saa 5 asubuhi
Wananchi wengi walijitokeza kushuhudia mchezo huo lakini wakakumbana na mabomu ya machozi baada ya jaribio la kuvunja geti ili waingie uwanjani
Kwa hakika itakuwa mechi ya kipekee na Mwananchi hakikisha umenunua tiketi yako mapema...!