Kocha Msaidizi wa Yanga Cedric Kaze amesema wameelekeza nguvu kuelekea mchezo wa ligi kuu dhidi ya KMC ambao utapigwa kesho Jumatano katika uwanja wa Benjamin Mkapa
Akizungumza katika Mkutano na Wanahabari, Kaze amesema hawakupata muda wa kufanya mazoezi baada ya mchezo dhidi ya TP Mazembe lakini wamefanya 'recovery', ari na morali za wachezaji ziko juu kuelekea mchezo dhidi ya KMC
"Tumefanya recovery nzuri baada ya mchezo dhidi ya TP Mazembe. Mechi mbili za CAF Confederation Cup zimetusaidia kuimarika, ari na morali ya wachezaji iko juu naamini watapambana ili kuweza kupata alama tatu"
"Tumekuwa na mwenendo mzuri katika mechi za ligi kuu zilizopita lakini hizo ni takwimu tu ambazo zinatupa heshima, kikubwa tunaangalia mechi iliyo mbele dhidi ya KMC"
"Mechi hii tunacheza katika nyakati ngumu kwa sababu mbele tunakabiliwa na mchezo wa kombe la Shirikisho lakini wakati huohuo tuko kwenye nyakati ambazo hatupaswi kupoteza alama kwenye ligi"
"Tumezungumza na wachezaji wasahau furaha ya matokeo ya mechi iliyopita na waelekeze nguvu kwenye mchezo muhimu dhidi ya KMC ambao tunapaswa kushinda," alisema Kaze
Akizungumzia hali ya kikosi, Kaze amesema hakuna majeruhi wapya, wachezaji watakaokosekana ni walewale ambao bado wako nje wakiendelea na matibabu akiwataja Benard Morrison, Denis Nkane na Aboutwalib Mshery