Ifikapo saa 1 usiku mabingwa wa soka Tanzania Bara Yanga watakuwa dimba la Benjamin Mkapa kuwakabili Real Bamako katika mchezo wa kombe la Shirikish, kundi D
Mchezo huo wa raundi ya nne hatua ya makundi, ni wa pili kwa Yanga kucheza kwenye uwanja wa nyumbani ambapo Wananchi watahitimisha mechi ya tatu nyumbani March 18 dhidi ya US Monastir
Yanga ilivuna alama tatu kwenye mchezo wa kwanza dhidi ya TP Mazembe, ushindi murua wa mabao 3-1
Mkakati wa Yanga ni kuvuna alama tisa nyumbani, ushindi katika mchezo wa leo dhidi ya Real Bamako utaongeza alama nyingine tatu
Kinachotizamwa na Wananchi ni kufuzu robo fainali ya michuano ya Shirikisho kwa mara ya kwanza Yanga ikiwa haijawahi kuvuka hatua ya makundi
Bila shaka Kocha Mkuu wa Yanga Nasreddine Nabi atashusha kikosi chake bora kama alivyofanya kwenye mchezo dhidi ya TP Mazembe na hata mechi iliyopita dhidi ya Real Bamako
Kiungo Khalid Aucho alipata majeraha kidogo katika mchezo dhidi ya Real Bamako uliopigwa Mali lakini imethibitishwa yuko timamu kushuka dimbani leo
Jesus Moloko pia alipata majeraha kwenye mchezo wa kombe la FA dhidi ya Tanzania Prisons lakini jana alishiriki mazoezi ya mwisho na wachezaji wenzake hivyo uwezekano ni mkubwa anaweza kutumika
Lakini kama Moloko atakosekana huenda Nabi akaanza na Stephane Aziz Ki au Tuisila Kisinda katika nafasi yake huku katika maeneo mengine akiwatumia wachezaji walewale walioipa Yanga ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya TP Mazembe
Jambo muhimu kwa Wananchi ni kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi uwanja wa Benjamin Mkapa leo ili kuwaongezea wachezaji hamasa
Shamrashamra zitaanza mapema tu uwanjani, saa 10 kuelekea kwenye mchezo wenyewe ambao utapigwa saa 1