Makamu wa Rais wa klabu ya Yanga Arafat Haji amewashukuru Wananchi waliojitokeza kwa wingi uwanja wa Benjamin Mkapa jana katika mchezo wa kombe la Shirikisho dhidi ya Real Bamako
Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 matokeo ambayo yamewaweka katika nafasi nzuri ya kutinga robo kama watashinda mchezo unaofuata dhidi ya US Monastir
Arafat amesema bado kazi haijamalizika, wanahitaji kuweka mkakati kabambe ili kuhakikisha wanashinda mchezo dhidi ya US Monastir March 19 katika uwanja wa Benjamin Mkapa, hii ndio mechi yao ya fainali kuelekea robo fainali
"Tumeshinda pamoja na kufikisha alama 7 lakini bado safari yetu hatujafika,Fainali yetu itakuwa Machi 19 watakapokuja wale walioshinda kwao mchezo wetu wa kwanza Us Monastir"
"Sisi viongozi wenu tunaingia msituni kuanzia sasa nanyi iwe hivyo kuanzia mechi za ligi na baadaye wapinzani wetu hawa,dhamira yetu hatutaki kuangusha alama nyumbani sisi sio wale"
"Sisi ndio Wananchi ambao ndio wenye nchi na ubora tutakaoendelea kuwa mfano wa kuchota mihela tofauti na wale wengine, tuna imani Mama zetu mmefurahi kwa Zawadi hii," aliandika Arafat kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii
Yanga inashika nafasi ya pili kundi D ikiwa na alama saba, alama tatu nyuma ya vinara US Monastir ambao tayari wametinga robo fainali
Kama itashinda mchezo unaofuata Yanga itafikisha alama 10 ambazo haziwezi kufikiwa na TP Mazembe wala Real Bamako