Yanga imeweka rekodi ya kushinda mechi 11 mfululizo katika ligi kuu ya NBC msimu huu
Ndio klabu ya kwanza kuweka rekodi hiyo katika historia ya ligi kuu ya Tanzania Bara
Ni timu iliyofanya maajabu mengi msimu huu. Kocha Mkuu Nasreddine Nabi amekuwa huru sana kufanya mabadiliko vile atakavyo katika kila mechi
Siku hizi kwenye kila mechi pale kikosi kinapowekwa hadharani husikii mashabiki wa Yanga wakihoji sana eti kwanini mchezaji fulani hayupo
Kwa sababu wanawaamini sana wachezaji wao, wote wapo katika kiwango bora na tayari kuipigania Yanga kila wanapohitajika
Nabi amefanya kazi kubwa kuiimarisha Yanga kimbinu lakini nyuma ya pazia yuko huyu mwamba Helmy Gueldich
Huyu ndiye msimamizi mkuu wa mazoezi ya fiziki ya wachezaji 'Fitnes coach'
Prof Helmy amemrahisishia kazi Nabi kwa kuwaweka wachezaji wote tayari kwa kutumika
Msimu uliopita kauli za Yanga kukata upepo kwenye kipindi cha pili zilisikika sana, msimu huu mmezisikia?
Yanga ya sasa usithubutu ukatangulia kuifunga, utajuta! Geita Gold ni mashahidi wa hili. Waulize nini kiliwakuta pale uwanja wa Azam Complex kwenye mchezo wa ligi kuu baada ya kutangulia kufunga kwenye kipindi cha kwanza
TP Mazembe, Real Bamako na hata US Monastir haikuwa bahati mbaya kwao kupigwa katika uwanja wa Benjamin Mkapa
Kwa sababu walikutana na timu ambayo wachezaji wake wameandaliwa vyema kimazoezi na Prof Helmy
Yanga inatabiriwa kufika mbali katika michuano ya kombe la Shirikisho barani Afrika wakiwa tayari wametinga hatua ya robo fainali
Prof Nabi na Cedric Kaze watasifiwa kwa kuiandaa timu yao kimbinu lakini Helmy atasifiwa kwa kuwafanya wachezaji wa Yanga wawe kama 'robot' kwani wako fit na hawachoki!





