Makamu wa Rais wa Yanga Arafat Haji amewataka Wanachama na Mashabiki wa Yanga kuendelea kuiunga mkono timu yao wakati wakiendelea kupanda mlima wa mafanikio
Jana Yanga ilivunja rekodi ya TP Mazembe kutofungwa kwenye uwanja wake wa nyumbani na klabu ya Tanzania baada ya Wananchi kuibuka na ushindi wa bao 1-0 huko Lubumbashi
Aidha Yanga ni kama imelipa kisasi cha matokeo ambayo TP Mazembe walipata dhidi ya Yanga kwenye michuano ya kombe la Shirikisho barani Afrika
Wananchi pia waliibuka na ushindi mabao 3-1 dhidi ya TP Mazembe katika mchezo wa kwanza uliopigwa uwanja wa Benjamin Mkapa
Arafat amesema ni wazi sasa Yanga inawatisha vigogo baada ya kumaliza vinara wa kundi D na sasa wanaelekeza nguvu kwenye mechi za robo fainali

"Awali ya yote kwanza kila mmoja kwa imani yake tumshukuru Mungu kwa kutufikisha siku ya leo ambayo Wananchi wanaendelea kufurahia mlima wa mafanikio tunaoendelea kuupanda"
"Tumemaliza hatua ya makundi kwa mafanikio makubwa ya kuongoza kundi letu D kwa kishindo kwa kufikisha jumla ya alama 13 lakini utamu zaidi ni ushindi wa ugenini tena dhidi ya timu kubwa Afrika TP Mazembe"
"Haya ni mafanikio ya umoja mkubwa ambao tunaendelea kuuishi ndani ya klabu yetu angalia jinsi viongozi wa juu walivyo wamoja lakini angalia wanachama na mashabiki wetu wanavyoishi kama familia"
"Yanga ilikuwa na matawi ndani ya nchi lakini Sasa rasmi mpaka nje ya nchi, Wananchi wenzetu wa Lubumbashi wametuonyesha kwa vitendo kwamba hii NI KLABU KUBWA AFRIKA NA DUNIANI. Hili vibe ambalo limeonyeshwa hapa Lubumbashi sisi viongozi wenu tunasema msimu huu hakuna wa kumuogopa mziki huu atapigwa yoyote"
"Ahsante sana viongozi wetu wa juu wa Baraza la Wadhamini Abbas Tarimba na Geofrey Mwambe lakini pia Lameck Nyambaya mjumbe wa Kamati ya Utendaji TFF kwa kujumuika nasi katika safari ya mchezo huu. Kipekee nimshukuru mfadhili wetu Ghalib Said Mohamed 'GSM' kwa uamuzi wake wa kushtua kusafiri na timu"
"Hawa watu watatu ukimuongeza na Rais wetu Injinia Hersi Said hakika wamekuwa zaidi ya hamasa kwa wachezaji wetu ambao leo wametupa heshima kubwa ya ushindi jadidi"
"Wananchi makundi yamekamilika Sasa tunarudi mechi za nyumbani tukiwasubiri CAF watuambie wanatuletea nani. Ikitokea Kuna mtu anakwambia Mazembe wepesi waulize wao waliwahi kuwafunga hata mara moja? Wakizidi kujipasua mishipa ya koo waulize watatupangia yupi Josh au Momo?," aliandika Arafat kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii